Mkuu wa Wilaya ya Ilala @mpogoloe amesema utunzaji wa mazingira ya Mlima Kilimanjaro ni jukumu la Watanzania wote, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anatunza mazingira pamoja na kupanda miti.
Amesema hayo leo 19, Juni 2024 wakati mkutano na waandishi wa habari kuzindua kampeni ya kuchangisha pesa kwaajili ya kampeni ya @Save_mt_kilimanjaro inayoendeshwa na Taasisi ya Nessa Foundation.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo alisema uhalisia wa Mlima huo ndio unaofanya kuvutia wengi kwenda kutembelea na kuongeza fedha za kigeni hivyo, Watanzania hawana budi kuungana kuokoa.
Alisema Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam itachangia sh milioni moja kwa ajili ya kununua miti na kuhimiza wadau wengine kujitokeza kusapoti kampeni hiyo ya Okoa Mlima Kilimanjaro kuchangia upatikanaji wa miti ya kutosha.
“Ukipanda Mlima wa Kilimanjaro utaona athari iliyotokana na moto, pia theluji imepungua tunatakiwa kuurudisha ule uhalisia wake, tunachofanya ni kushirikiana na Nessa Foundation na Tanapa katika kampeni huu ili kuuokoa,”alisema
Wakati anaitambulisha harambee hiyo, Mkurugenzi wa Nessa Deborah Nyakisinda, alisema matembezi hayo yatafanyika Julai 20, mwaka huu na kuongozwa na mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Philip Mpango.
Nyakisinda alisema miti inayohitajika kwa ajili ya kurejesha uhalisia wa mlima huo ni bilioni moja na kuwahimiza wadau kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono.
“Ni wajibu wa kila mmoja kuulinda mlima huu sio kwa watu wa Kilimanjaro pekee yake bali Watanzania wote kwa kuwa ni mlima wetu sote,”alisema
Naye Mhifadhi Mkuu Mfawidhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) Hassan Nguluma alihimiza jamii inayozunguka Mlima Kilimanjaro umuhimu wa kulinda mazingira ya mlima huo.
Wengine walioahidi kuchangia kampeni hiyo ni Mfuko wa @utt sh milioni tatu huku benki ya Maendeleo ikiahidi kuchangia miti 50.
Matembezi yatakuwa ya km 5, 10 na 16 kuanzia geti la Marangu hadi Mandara.