Mkuu wa Wilaya ya Pangani kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Utalii nchini wameandaa mafunzo Maalum ya muda mfupi kwa Vijana wa Pangani likiwa ni kuwaandaa Vijana kuweza kukidhi ushindani kwenye Soko la ajira hasa ukizingatia kuwa Pangani ni Mji wa Utalii.
DC Zainab amesema mafunzo hayo yatawasaidia Vijana wa Pangani kutambua fursa zilizopo katika Sekta ya Utalii na kuwa tayari kwa uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa Hoteli kubwa za kisasa kwenye fukwe za Pangani.
Mafunzo yameanza na Vijana 50 ambapo Vijana 20 watakaofanya vizuri kwenye mafunzo haya watapatiwa “Samia Tourism Scholarships” ili waweze kusoma mafunzo ya mda mrefu kwenye Chuo cha Taifa cha Utalii.
Mafunzo haya yanaendana sambamba na kampeni ya “Wekeza Pangani” ambayo inalenga kuwakaribisha Wawekezaji na Wafanyabiashara ndani na nje ya Nchi kuja kuwekeza Pangani.
DC Zainab amesema kwa sasa Agenda ya Uchumi ndio kipaumbele kwa Watu wa Pangani, na sekta za kipaumbele ni Utalii, Kilimo biashara na Uchumi wa Buluu. Pangani ipo karibu na Zanzibar, Mombasa, Dar es salaam na Kanda ya Kaskazini. Hivyo kila aliye tayari kuwekeza basi Pangani ni mahala salama na sahihi kuwekeza.