MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni, amewataka wasimamizi wa miradi inayoendelea kujengwa ndani ya wilaya hiyo kushirikiana na maafisa wa serikali wanapofanya ziara za ukaguzi.
Amesisitiza kuwa ziara hizo zina lengo la kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia ubora, thamani ya fedha, na kasi inayotakiwa ili kuepusha ubadhilifu na ujenzi wa majengo yasiyo na viwango stahiki.
Kasilda alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akikagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Kata ya Hedaru, katika ziara hiyo aliambatana na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Same ambapo alibainisha kuwa maafisa wa serikali na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi ya Wilaya wanapokagua miradi, wanakuwa na nia njema ya kushauri na kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa viwango vilivyokusudiwa.
“Katika miradi yote inayoendelea wilayani hapa, nawasihi wasimamizi wa miradi kutoa ushirikiano kwa maafisa wa serikali pale watakapoona changamoto, watawashauri ili kuhakikisha mradi unakuwa bora na unakidhi viwango vinavyotakiwa,” alisema Kasilda.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutunza nyaraka za miradi ili viongozi wanapofanya ukaguzi waweze kuona uwiano kati ya fedha zilizotolewa na kazi inayoonekana pia alihimiza ukaguzi wa vifaa vinavyopokelewa ili kuhakikisha ubora wake katika utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Same, Daimon Mwakababu, aliwataka wasimamizi wa miradi, viongozi wa siasa, na serikali kutoingilia majukumu ya TAKUKURU.
Alisisitiza kuwa taasisi hiyo haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa miradi au kujihusisha na vitendo vya ubadhilifu.
“Ili fedha za serikali zitumike ipasavyo, nawasihi watumishi wa umma wanaosimamia miradi pamoja na viongozi wa siasa kutoingilia kazi za TAKUKURU tuacheni tufanye kazi kama alivyoagiza Rais hatutasita kumchukulia hatua yeyote atakayejihusisha na uhalifu wa aina yoyote,” alisema Mwakababu.