SERIKALI imesisitiza dhamira yake ya kutumia mbio za NBC Dodoma Marathon kama chanzo cha kuwapata wanariadha sahihi watakaoliwakilisha Taifa kwenye mashindano ya kimataifa yakiwemo mashindano ya Olympic na Mashindano ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth).
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro amebainisha hayo jijini Dar es Salaam leo Jumatatu huku akithibitisha nia yake ya kukimbia km 42 (full marathon) kwenye mbio hizo zinatotarajiwa kufanyika jijini Dodoma, tarehe 28 Julai mwaka huu.
Lengo kuu la mbio hizo zinazotarajiwa kuongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ni kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga ili kuboresha afya ya mama wa mtoto.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya benki ya NBC akiwa sambamba na mwenyeji wake Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi, Dk. Ndumbaro alipongeza jitihada za benki hiyo katika kuinua sekta ya michezo nchini.
Alisema kwa sasa Taifa linakabiliwa na uhaba mkubwa wa wanariadha wenye sifa ya kushiriki mashindano ya kimataifa hivyo serikali imejipanga kutumia mbio hizo kutambua wanariadha wenye sifa sahihi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano mbalimbali ya kimataifa.
“Kwa sasa kwenye mashindano ya Olympic tunakwenda na wanariadha wachache sana kwasababu hatuna maandalizi ya kutosha. Hivyo NBC Dodoma Marathon ni moja ya chanzo cha kupata wanariadha wazuri ili baada ya mbio hizi tuweze kuwatamuba na kuwapa mafunzo zaidi ili mashindano ya ‘Commonwealth’ na Olympic na mengine mbalimbali ya kimataifa tuwe na wanariadha wengi zaidi,” alibainisha Dk. Ndumbaro.
Aidha, Dk. Ndumbaro aliipongeza benki hiyo kwa jitihada mbalimbali za kuendeleza sekta ya utamaduni, sana ana michezo kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo udhamini wa michezo na huduma za kibenki zinazolenga kuwasaidia wadau mbalimbali wa sekta hizo.
“Tofauti na mbio hizi, jitihada za benki ya NBC kwenye kuinua sekta ya michezo zinaonekana kupitia udhamini wake kwenye ligi za NBC Premier League, NBC Championship na NBC Youth league ambapo imewekeza kiasi cha Sh. 32.6 bilioni kwenye ligi hizo.
“Pia NBC inashiriki katika uwezeshaji kiuchumi kwa wasanii kupitia mfuko wa maendeleo ya sanaa nchini sambamba na kusimamia kamati ya Hamasa ya Timu za Taifa ambapo mpaka sasa imeshakusanya kiasi cha Shilingi 2 bilioni kati kutokana na ahadi za awali za Sh.4 bilioni zilizopokelewa katika hafla ya uzinduzi wa kamati hiyo,” alisema.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Sabi alisema jitihada za benki hiyo katika kuendeleza sekta ya michezo nchini kwa kiasi kikubwa inachagizwa na imani ya benki hiyo kuwa sanaa na michezo ni nguzo ya ajira na kuunganisha taifa.
“Kwa mfano kupitia udhamini wetu kwenye ligi tatu muhimu za mpira wa miguu hapa nchini, mbali na kuzalisha vipaji tumezalisha ajira za moja kwa moja zaidi ya 7,000 na mamilioni ya ajira zingine kwenye mnyororo wa uchumi. Zaidi pia kupitia mbio hizi za NBC Dodoma Marathon kwa kushirikiana na wadau wetu mbalimbali tunalenga kukusanya fedha kusaidia juhudi za Serikali katika kuboresha ya afya ya mama na mtoto kupitia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na kutoa ufadhili kwa wakunga,” alisema.
Mwisho.
Captions
PIC 1
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro (kushoto) akipokea sweta maalum la mbio za NBC Dodoma Marathon kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi ikiwa ni ishara ya kumkaribisha rasmi Waziri huyo kwenye mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Julai 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma zikiwa na lengo la kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga ili kuboresha afya ya mama wa mtoto Makabiziano hayo yamefanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam leo.