Hatimaye Sean “Diddy” Combs ameikosa dhamana kwa mara ya tatu kutoka kwa hakimu katika jiji la New York.
Majaji wawili hapo awali walikataa kuachiliwa kwa Bw.Combs kutoka kizuizini, haswa kwa sababu ya wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuchezea mashahidi, wakiona kuwa ni hatari kubwa ikiwa ataachiliwa kabla ya kesi, ambayo imepangwa Mei 2025.
Bwana Combs anazuiliwa katika Kituo cha Kizuizi cha Metropolitan huko Brooklyn, New York, akishtakiwa kwa kula njama, biashara ya ngono na usafirishaji kwa shughli za ukahaba.
Amedai kutokuwa na hatia na pia amekanusha zaidi ya dazeni mbili za tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia zilizowasilishwa katika msururu wa kesi za madai.
Hakimu alitoa ushahidi katika kesi hiyo unaoonesha madai ya Bw Combs kuingilia ushahidi, ukiukaji wake wa kanuni za gereza akiwa gerezani na madai kwamba aliendesha “biashara ya uhalifu” ikiwa ni pamoja na kazi ya kulazimishwa na utekaji nyara.
Jaji wa Wilaya ya Marekani Arun Subramanian alihitimisha mahakama haiwezi kumwamini Bw Combs ikiwa angeachiliwa kwa dhamana.
“Mahakama inaona kwamba serikali imeonesha kwa ushahidi wa wazi na wa kuridhisha kwamba hakuna masharti au mchanganyiko wa masharti yatahakikisha usalama wa jamii,” jaji aliandika katika uamuzi wa Jumatano.
Waendesha mashtaka walikuwa wamepinga kumpa Bw Combs dhamana, wakitaja utovu wa nidhamu wake akiwa kizuizini.