Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema pamoja na mambo mengine, dira mpya ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2050 itaijenga Tanzania kuwa taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea.
Prof. Kitila ameeleza hayo mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi tarehe 11 Desemba 2024 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo iliyofanyika Zanzibar
Waziri Kitila amesema kuwa kufikia mwaka 2050, Tanzania inatakiwa kuwa imeingia kwenye nchi za kipato cha kati ngazi ya juu ikichagizwa na sekta ya uzalishaji viwandani, ili kufikia pato la mtu mmoja la Dola za Marekani 4700 huku pato la taifa likitarajiwa kufikia Dola za Marekani Bilioni 700.
Aidha kulingana na Waziri Kitila, Dira 2050 imenuia pia kuondoa umaskini uliokithiri na kupunguza umaskini wa mahitaji ili kuwa chini ya asilimia 5 kutoka asilimia 26 ya hivi sasa.
Katika hatua nyingine akieleza shabaha nyingine ya Dira 2050, Prof. Kitila Mkumbo amesema Tanzania imedhamiria kuwa kinara wa uzalishaji wa chakula barani Afrika pamoja na kuwa wazalishaji wakubwa kumi wa chakula duniani.