Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga, Thomas Masese, amewakumbusha wafanyabiashara kuhusu dirisha la makadirio ya kodi kwa mwaka wa 2025, linaloanzia Januari hadi Machi 2025, likiwa na lengo la kurahisisha ulipaji kodi bila kuwekewa adhabu.
Akizungumza Meneja Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga amesema kuwa lengo la kukutana na wadau hao ni katika kujenga mahusiano mazuri na wadau mbalimbali, hususan wafanyabiashara, watu wenye mahitaji maalum, na viongozi wa makundi mengine, katika jitihada za kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kuukaribisha mwaka mpya wa 2025.
Aidha Bw.Masese ameongeza kwa kusema kuwa katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2024, TRA imekusanya kiasi cha TZS bilioni 178.3, ambacho ni zaidi ya lengo lililowekwa la TZS bilioni 162, ikiwakilisha ufanisi wa asilimia 109 na ametoa shukrani kwa walipa kodi kwa mchango wao.
Hatahivyo Masese amesema kuwa “suala la usalama, niwaombe wananchi kuwa na tahadhari kuhusu watu wanaojitambulisha kama maafisa wa TRA na wale wenye mashaka kufika ofisi za TRA au kuwasiliana na viongozi wa mamlaka hiyo badala ya kutumia nguvu au kuwashambulia maafisa hao”
Naye Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Tanga, Rashidi Mwanyoka,akatoa Maoni yake kwa Niaba ya Viongozi wa Wafanyabiashara
ameonyesha ushirikiano wao mzuri na TRA kwa kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari, akisisitiza umuhimu wa kodi katika kuendeleza miradi ya maendeleo ya Serikali.