Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametembelea na kukagua ujenzi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga Mkoani Rukwa ambao unasimamiwa na TANROADS chini ya mkandarasi Beijing Construction Engineering Company Ltd.
Katika ukaguzi wa ujenzi huo, Balozi Dkt. Nchimbi ameambatana na Katibu wa NEC – Itikadi, Uenezi na Mafunzo Ndg. Amos Makalla na Katibu wa NEC – Oganaizesheni Ndg. Issa Haji Gavu.
Akipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa Meneja wa TANROADS mkoa wa Rukwa Bi. Mgeni J. Mwanga, amemueleza Katibu Mkuu kuwa mkataba wa kuanza kwa ujenzi huo ulisainiwa Aprili, 2023 ambapo ujenzi unatakiwa kukamilika ndani ya miezi 18 (kuamilika Oktoba, 2024).
Pia, amebainisha kuwa gharama ya mradi huo ni Tsh Bilioni 60.1 na hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 8% ambapo kimkataba ilipaswa kuwa asilimia 15% na kueleza Jengo la abiria linalojengwa litakuwa na uwezo kuchukua abiria laki 150,000 na litakuwa la ghorofa mbili na kubainisha kuwa hadi sasa zimezalishwa ajira 120 zikiwemo 114 za watanzania na 9 ni wanawake ambapo amesema wanatarajia kuongeza wanawake wengine.
Mara baada ya kupokea tarifa hiyo, Balozi Dkt. Nchimbi amesema kiwanja hiko ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya usafiri na uchukuzi na kimesubiriwa kwa muda mrefu na wakazi wa Mkoa wa Rukwa na kumtaka mkandarasi huyo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ndani ya muda wa kimkataba na ukamilike ukiwa na ubora.
Balozi Dkt. Nchimbi ametoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kufanya maamuzi mazuri ya kujenga uwanja huo wa ndege kwakuwa itatua changamoto ya usafirishaji wa anga.
Maboresho yanayofanyika ni pamoja na ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege (Runway) yenye urefu wa Km 1.75, ujenzi wa barabara ya kiungio (Taxiway) na ujenzi wa maegesho ya ndege (Apron), Ujenzi wa Jengo la abiria (terminal building), usimikaji wa mifumo ya taa za kuongozea ndege (airfield ground lighting system) pamoja na alama(aerodrome signage).
Vilevile, Mkandarasi atafanya ujezi wa uzio wa usalama na barabara za kuzunguka uzio wa uwanja na ujenzi wa jengo la kuongozea ndege( Air Traffic Control Tower).