Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezitaka Mamlaka za Udhibiti na Ununuzi wa Umma Afrika Mashariki kuzingatia weledi, maadili na uwajibikaji ili kuleta ufanisi uliokusudiwa.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Jukwaa la 16 la Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) lililofanyika leo Septemba 9, 2024 jijini Arusha.
Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali zinatambua kwamba fedha nyingi zinazotengwa kwenye bajeti kila mwaka zimekuwa zikitumika kupitia ununuzi wa umma. Kwa kuzingatia hilo, Serikali imekuwa makini kuhakikisha kuwa fedha hizo kupitia ununuzi wa umma zinapata usimamizi makini.
Ambapo kupitia kifungu cha 7 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura ya 410 ya Mwaka 2023, Serikali imeipa Wizara ya Fedha jukumu la kuhakikisha inaandaa Sera ya Taifa na Mkakati wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ili kuhakikisha ununuzi na shughuli zote zilizofunganishwa katika mnyororo wa ugavi zinazofanyika kwenye taasisi za umma zinazingatia sera hiyo na mikakati itakayowekwa.
“ Naomba Waziri wa Fedha mlisimamie hili na haya ni maelekezo ya Mhe. Rais. Kupitia majukwaa yaliyofanyika yote yametilia mkazo maadili, weledi, uwazi na uwajibikaji na bila maadili wananchi hawezi kupata huduma, pia fedha nyingi zinazotengwa kwa ajili ya wananchi kupata huduma zinaamriwa na kundi hili na kama hatuna taasisi imara za ugavi na ununuzi hatutapata matokeo ya fedha na hatimaye umasikini utaongezeka,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “Nawaomba mnapojadili leo mkumbushane umuhimu mkubwa wa kulinda taaluma yenu, ioneeni wivu isimamieni taaluma yenu akitokea mtu anafanya vitendo visivyofaa mkemeeni. Jisimamieni wenyewe, asitokee mtu katikakati ya manunuzi anataka kufanya vitendo visivyofaa, PPRA simamieni vizuri jambo hili ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.
Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali ya Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kisheria katika ununuzi wa umma ambayo yalianza mwaka 2001 kwa kutungwa kwa Sheria ya kwanza ya Ununuzi wa Umma. Baada ya changamoto kadhaa, zilipelekea mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2004, na kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
“Serikali kupitia PPRA kama chombo cha Udhibiti wa Ununuzi wa Umma ililenga kufanya mageuzi na kuboresha usimamizi wa ununuzi wa umma, kuhakikisha thamani ya fedha, uwazi, na uwajibikaji, ufanisi na uadilifu katika ununuzi na ugavi na kujenga uwezo katika ununuzi na ugavi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amebainisha Dkt. Biteko.
Ametaja maboresho yaliyofanywa na Serikali kuwa ni kuboresha mfumo wa kisheria na kuweka miundo ya utawala, uboreshaji wa mifumo ya kidijitali, kuajiri na kuwajengea uwezo wafanyakazi, kuboresha upatikanaji wa zabuni kwa Watanzania ambapo ametolea mfano kuwa wazawa wakijengewa uwezo wanaweza kufanyakazi vizuri hata nje ya nchi, pamoja na kuimarisha vita dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Pia, Dkt. Biteko amesema kuwa Mamlaka zote za Ununuzi wa Umma kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaoshiriki kwenye Jukwaa hilo nao wana malengo yanayofanana na Tanzania.
“Kutokana na malengo ya uanzishwaji wa mamlaka hizi, natoa wito kwa Mamlaka zote kuhakikisha kuwa mnasimamia malengo mliyoyaweka ili kuhakikisha tija na ufanisi unapatikana katika usimamizi wa sekta hii ili huduma kwa wananchi iendelee kupatikana kwa wakati na kwa ufanisi,” amebainisha Dkt. Biteko.
Amesisitiza “Tunapotumia fedha za umma kununua bidhaa, huduma au miradi katika nchi zetu, tunapaswa pia kufahamu hitaji la maendeleo endelevu na ustawi wa ushirikiano baina ya nchi zetu za Afrika Mashariki. Hii ina maana kwamba, mifumo yetu ya ununuzi kwa nchi za Afrika Mashariki inapaswa kuhakikisha inajengwa kwa lengo la kuleta manufaa ya muda mrefu kwa wananchi wetu.”
Akizungumzia mfumo wa NeST, Dkt. Biteko amefurahishwa na mfumo huo kujengwa na vijana wa Kitanzania ambao nchi nchi nyingi za Afrika Mashariki zimeanza kuutamani mfumo huo ambao umekuwa na faida za kupunguza gharama za kufanya ununuzi kwa wazabuni wa Serikali, kuondokana na matumizi ya karatasi, kuongezeka kwa kasi ya ununuzi pamoja na kupunguza makosa katika ununuzi na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amewapongeza washiriki kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushiriki jukwaa hilo ambao kupitia jukwaa hilo watapata fursa ya kubadilishana ujuzi na uzoefu pamoja na kujadili masuala muhimu yanayohusiana na ununuzi wa umma kwenye nchi za Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad H. Chande ameipongeza Serikali kwa kuendelea kufanya maboresho mbalimbali katika sekta tofauti tofauti nchini ikiwemo sekta ya ununuzi wa umma ambao umeonesha kuwa na tija katika sekta hiyo.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El Maamry Mwamba amesema kuwa Jukwaa hilo linalenga kuwakutanisha wadau kuzungumzia masuala ya ununuzi wa umma kwa manufaa ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa mwaka 2024 linafanyika nchini Tanzania na kuandaliwa na Wizara ya Fedha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Dkt. Leonada Mwagike ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa kufanya maboresho makubwa katika sekta ya ununuzi wa umma na kuleta tija ya kuongeza uwajibikaji ili kupata thamani halisi ya fedha inayoonekana.
Dkt. Mwagike ameahidi Mamlaka hiyo kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali ili Watanzania wapate huduma bora.
“ Ili kuonesha ufanisi katika ununuzi wa umma Serikali ilianza kutumia Mfumo wa Elektroniki wa Ununuzi wa Umma na baadae kujiunga na Mfumo wa NeST na kuanza kutumika 2023 ambao umejengwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo eGA,” ameeleza Dkt. Mwagike.
Amesema kuwa Mfumo huo unasomana na taasisi 17 ya mifumo ya Serikali ikiwemo Benki Kuu, CRB, OSHA, TIRA, PeG kwa kuzingatia maelekezo mahsusi ya Mhe. Rais ya kuhakikisha mifumo inasomana.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba amesema kuwa majukwaa hayo hukutana kupitia nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo huwa na majadiliano na maazimio na katika Jukwaa la 16 washiriki watapata fursa ya kuangalia utekelezaji wa maazimio ya jukwaa la 15.
“Kupitia mada mbambali washiriki watapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa namna teknolojia inavyoweza kuongeza ufanisi katika ununuzi wa umma na kusaidia nchi wananchama kuboresha ununuzi wa umma na kushughulikia changamoto zilizopo katika ununuzi wa umma.” Amesema Bw. Simba.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Ndomba ametaja moja ya jukumu la taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kusimamia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa umma na inatambua kuwa ununuzi wa umma nchini ni eneo linalohitaji kusimamiwa vizuri ili kuleta matokeo tarajiwa.
Mhandisi Ndomba ameongeza kuwa sambamba na kusimamia mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Uendeshaji Shehena na Mfumo wa Malipo Serikalini (GePG), eGA inasimamia pia Mfumo wa ununuzi wa NeST.
“ Hadi sasa mifumo 164 imeshaunganishwa na kuwezesha kubadilishana taarifa ili kuongeza ufanisi, pia tunahamasisha taasisi zingine zijuinge na mfumo huu ili kuongeza tija ya utendaji.” Amemaliza Mhandisi Ndomba.
Awali Dkt. Biteko amepokea tuzo aliyotunukiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuboresha sekta ya ununuzi wa umma nchini. Aidha tuzo ingine imetolewa kwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, Benki ya NMB, Stanbik na TCB, Tanzanine Corporates, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, Suma JKT, BRELA.
Taasisi zingine zilizopewa tuzo ni eGA, Shirika la Mzinga, GPSA, TANESCO na Benki ya Maendeleo ya Kilimo, ISUZU, MSD, Kampuni ya Mtandao wa Simu ya TIGO, Chuo cha Uasibu Arusha, Superdoll, TANROADS, CRDB, NSSF, TRA, Ando, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, TMA, Clouds Media Group, AICC.
Jukwaa hilo la 16 limeongozwa na kauli mbiu inayosema “Utumiaji wa Mifumo ya Kielektroniki kwa Ununuzi wa Umma Endelevu”