Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo, amezihimiza taasisi za kilimo nchini kubadili mbinu za utendaji kwa kuachana na mazoea na badala yake kuimarisha matumizi ya utaalamu katika kuwawezesha wakulima kuongeza tija na kuendesha kilimo cha biashara.
Dkt. Diallo alitoa wito huo tarehe 19 Februari 2025, katika siku ya pili ya ziara ya Bodi na Menejimenti ya TFRA walipotembelea taasisi mbalimbali za Wizara ya Kilimo, ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI – Maruku), Kituo cha Uhaulishaji Teknolojia za Kilimo (MATI – Maruku), na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI). Ziara hiyo inalenga kuelewa majukumu ya taasisi hizo na kuimarisha ushirikiano katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea miongoni mwa wakulima.
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Diallo amesisitiza kuwa ili kufanikisha malengo ya serikali kupitia kauli mbiu ya Agenda 10/30: Kilimo ni Biashara, wataalamu wa kilimo wanapaswa kuongeza jitihada katika kutoa elimu na ushauri kwa wakulima ili kubadili mitazamo hasi kuhusu matumizi ya mbolea na kuchochea uzalishaji wenye tija kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Bw. Joel Laurent, ameeleza kuwa, ziara hiyo imetoa fursa kwa TFRA kufahamu kwa undani zaidi shughuli za taasisi hizo na kutathmini maeneo ya ushirikiano ili kuongeza ufanisi katika uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea.
Amebainisha kuwa TFRA inajumuisha wakufunzi wa MATI katika programu zake za mafunzo kwa wakulima, ili kuwawezesha wakufunzi hao kuendeleza utoaji wa elimu kwa wakulima kwa ufanisi pindi mafunzo yanapohitajika.
Katika wasilisho lake, Meneja wa TARI – Maruku, Dkt. Mpoki Shimwela, ameeleza kuwa, matumizi duni ya mbolea katika kilimo cha migomba yamesababisha upungufu wa virutubisho kwenye udongo, hali inayochangia kuzalisha ndizi kilo chache na zisizo na ubora unaokidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa
Alibainisha kuwa, TARI imeanzisha miradi mbalimbali ya kuhamasisha matumizi ya mbolea, ikiwa ni pamoja na vipimo vya afya ya udongo kwa wakulima ili kuwasaidia kuelewa mahitaji halisi ya udongo wao.
Shaban Mkulila, mkulima wa kahawa kutoka Kijiji cha Maruku, baada ya kutembelewa na Bodi na menejimenti ya TFRA shambani kwake Maruku ameeleza kuwa, tangu aanze kutumia mbolea katika kilimo cha kahawa mwaka 2019, ameshuhudia ongezeko kubwa la mavuno.
Ameishauri TFRA kuanzisha mashamba darasa ili wakulima wapate mafunzo kwa vitendo na kuwasaidia kuondokana na dhana potofu kwamba mbolea inaharibu udongo.
Naye, Bw. Siraji Amri, mkulima wa kahawa kutoka Kijiji cha Mulata, Kata ya Katerero, amethibitisha kuwa matumizi ya mbolea za viwandani yamemwezesha kuongeza uzalishaji hadi kufikia wastani wa kilo sita za kahawa kwa kila mti mmoja, hali inayothibitisha mchango wa mbolea katika kuimarisha tija ya kilimo.
Ziara hiyo imetoa mwangaza kuhusu umuhimu wa ushirikiano kati ya TFRA na taasisi za kilimo katika kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi kuhusu matumizi ya mbolea kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na kufanikisha azma ya kilimo biashara nchini.