Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo tarehe 8 Oktoba, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Hungary, Mhe. Tamas Sulyok katika Ikulu ya nchi hiyo iliyopo Jijini Budapest.
Katika mazungumzo yao, Viongozi hao walijadili njia bora za kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa haya mawili, Tanzania na Hungary, katika sekta mbalimbali hususani kilimo, utalii, biashara na maji. Rais Sulyok alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Dkt. Tulia kwa juhudi zake za dhati katika kuendeleza amani duniani, hususani katika maeneo yanayokumbwa na migogoro mikubwa.
Aidha, walizungumzia pia masuala yanayohusu misingi na malengo ya IPU, ambapo Mhe. Sulyok aliahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza ajenda zote za IPU.
Ifahamike kuwa kati ya nchi nane zilizounga mkono kuanzishwa kwa IPU katika mkutano uliofanyika tarehe 29 na 30 Juni 1889 nchini Ufaransa, Hungary ilikuwa miongoni mwao, sambamba na Uingereza, Ufaransa, Marekani, Denmark, Ubelgiji, Uhispania na Liberia kutoka Afrika. Hii ndio sababu Hungary inaadhimisha miaka 135 ya kuanzishwa kwa IPU.