Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amechangia pesa zake binafsi, Tsh. Milioni 70 kusaidia Watoto njiti kupitia Taasisi ya Doris Mollel Foundation ambapo ameingiza Milioni 20 kwenye akaunti ya Doris Mollel Foundation na amenunua pia vifaa vya kuwasaidia Watoto Njiti vyenye thamani ya Tsh. Milioni 50.
Wakizungumza kwenye mahojiano maalum ya pamoja na Ayo TV katika Hifadhi ya Serengeti leo, Naibu Waziri wa Afya Dr. Godwin Mollel, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja na DC wa Serengeti Dr. Vicent Mashinji wamempongeza na kumshukuru Rais Samia kwa msaada wake huo na kusema Serikali kwa ujumla inaendelea kufanya mambo mengi kuwasaidia Watoto njiti kwa kushirikiana na Wadau kama Doris Mollel Foundation.
Taasisi ya Doris Mollel Foundation leo ikiongozwa na Mkurugenzi wake Doris Mollel imeadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani ambayo kwa kawaida huadhimishwa mnamo tarehe 17 Novemba kila mwaka, kwao maadhimisho hayo yamefikia kilele leo November 20, 2022 ambayo ni Siku ya Mtoto Duniani na yanafanyika katika viwanja vya Robanda, vilivyopo katika Wilaya ya Serengeti, Mkoani Mara kwa kugawa vifaa tiba na kufanya utalii katika Hifadhi ya Serengeti ikiwemo kupanda Hot Air balloon na kutalii katika Hifadhi ya Serengeti kwa ajili ya kukuza utalii na kuhamasisha kujitolea.