Dozi Elfu 10 za Mpox za kwanza zinatarajiwa kuwasili barani Afrika Kuanzia wiki hii, wakati huu pia maambukizo zaidi yakiendelea kuripotiwa hali iliyofanya shirika la afya duniani kutangaza ugonjwa huu kama janga la kidunia.
Chanjo hizo zinaletwa Afrika baada ya mataifa zaidi ya 70 nje ya Afrika kuwa nazo, dhihirisho kuwa mafunzo kutokana na uviko 19 ambapo Afrika ilibaguliwa katika usambazaji wa chanjo ,bado hayajaweza kuleta mabadiliko.
Kwa mujibu wa taasisi ya kudhibiti magonjwa barani ,Afrika CDC, ucheleweshaji huu ambao umelazimu Afrika kutegemea chanjo za msaada ni kuwa sababu kampuni za kuzalisha chanjo zilihitaji kupata idhini kutoka WHO ,idhini ambayo imetolewa mwezi huu .
Kufikia sasa kuna aina mbili za chanjo ,moja inayotengenenezwa na kampuni ya Denmark ya Bavarian Nordic inayogharimu dola mia moja kwa dozi ,na ile inayozalishwa na kampuni ya Japan KM Biologics ambayo bei yake bado haifahamiki.
Afrika kwa mujibu wa CDC ina uhitaji wa dozi milioni kumi ,na imekuwa na dozi laki mbili ,DRC ambayo imeathirika zaidi na mpox ikiwa kipau mbele.