Baraza Kuu la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (CENCO) liliamua, siku ya Jumamosi, Desemba 23, kwamba Kanisa Katoliki la DRC halitabariki ndoa ya wapenzi wa jinsia moja.
Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini DRC walieleza msimamo wao kufuatia barua ya papa iliyowaidhinisha makasisi kutekeleza baraka rahisi, nje ya liturujia, ya ndoa ya wapenzi wa jinsia moja.
Katika mahojiano na Radio Okapi, Jumapili hii, Desemba 24, katibu mkuu wa CENCO, Askofu Donatien Nshole alifafanua kuwa CENCO haimpingi Papa Francis. Hakika, barua kutoka kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani inatoa uhuru kwa maaskofu kutathmini, kwa kuzingatia hali halisi ya kijamii na kitamaduni ya makanisa ya ndani, kama baraka hii rahisi inaweza kufanywa au la ndani ya jumuiya zao za kikanisa, alieleza Askofu Donatien Nshole.
Hivyo kwa CENCO, katika muktadha wa Kongo, kubariki ndoa ya wapenzi wa jinsia moja kuna hatari ya “kudhoofisha imani” ya baadhi ya Wakristo, aliongeza Askofu Nshole.
Kulingana na Baraza Kuu la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini DRC, ndoa ipo kati ya mwanamume na mwanamke pekee na kwa kawaida iko wazi kwa uzazi.