Takriban watu 10 wameuawa na idadi isiyojulikana ya wengine kutekwa nyara mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na waasi wenye itikadi kali wanaohusishwa na kundi la Islamic State, msemaji wa jeshi alisema Jumatatu.
Waasi wa Allied Democratic Forces (ADF), tawi la IS katika eneo hilo, walishambulia eneo la Batangi-Mbau katika jimbo la Kivu Kaskazini Jumapili usiku, kulingana na msemaji Mak Hazukay. Nyumba kadhaa zilichomwa moto wakati wa shambulio hilo, aliongeza.
“Tunatoa wito kwa wakazi kuwa waangalifu na tunawahakikishia kwamba tutamfukuza adui nje ya eneo letu,” Hazukay alisema.
Mashariki mwa DRC imekumbwa na ghasia za kutumia silaha kwa miongo kadhaa, huku zaidi ya makundi 120 yakipigania mamlaka, ardhi na rasilimali muhimu za madini, huku wengine wakijaribu kutetea jamii zao. Baadhi ya makundi yenye silaha yameshutumiwa kwa mauaji.
Ghasia hizo zimewalazimu karibu watu milioni 7 kukimbia makazi yao.