Shirika la afya duniani WHO, limewalipa wanawake 104 waathiriwa dhulma za kingono nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo fidia ya Dola 250 kila mmoja .
Kwa mujibu wa ripoti kutoka WHO, daktari Gaya Gamhewage ,kutoka kitengo cha kupambana na dhulma za kingono,katika shirika hilo, alisafiri kwenda DRC mwezi Machi kulishughulikia swala hilo ambapo wafanyikazi wa WHO waliokuwa wakisaidia kupambana na mlipuko wa Ebola wanatuhumiwa kuwanyanyasa kimapenzi wanawake hao 104.
Daktari Gaya katika ripoti yake kwa UN kuhusu ziara yake, amesema alikutana na wanawake hao, mmoja wao akiwa amejifungua mtoto aliyekuwa na matatizo ya kiafya na kuhitaji kugharamika zaidi kupata matibabu maalum.
Wadadisi wamehoji kiasi hicho kilicholipwa na WHO kilikuwa kidogo ikilinganishwa na gharama ya safari ya daktari Gaya ya siku tatu.
WHO kabla kufanya malipo hayo,iliwasajili wanawake hao katika mafunzo ya kujifunza namna ya kujishughulisha na kupata kipato ,ingawaje wengi wa akina mama waliodhalilishwa kimapenzi waliachwa nje ,WHO ikisema wengi wao walikataa ofa hiyo, asilimia kubwa wakiwa hawajulikani waliko.