Maafisa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesema dozi 50,000 za chanjo dhidi ya Mpox kutoka Marekani ziliwasili Jumanne, wiki moja baada ya shehena ya kwanza kutoka Umoja wa Ulaya kuwasili nchini humo.
Watu wazima huko Equateur, Kivu Kusini na Sankuru, majimbo matatu yanayoathirika zaidi, ndio watapewa chanjo hiyo kwanza, kuanzia tarehe 2 Oktoba, Cris Kacita Osako, mratibu wa kamati ya Congo ya kukabiliana na Monkeypox, aliiambia AP.
Wiki iliyopita, shehena ya kwanza ya chanjo ya mpox iliwasili katika mji mkuu wa DRC, kitovu cha mlipuko huo.
Dozi 100,000 aina ya JYNNEOS zilizotengenezwa na kampuni ya Denmark, Bavarian Nordic, zilitolewa kama msaada na Umoja wa Ulaya kupitia idara yake ya majanga ya afya (HERA).
Dozi nyingine 100,000 zilitolewa mwishoni mwa Juma.