Makubaliano hayo yamepitishwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kati ya vyama vinavyounga mkono serikali na baadhi ya vyama vya upinzani pamoja na baadhi ya mashirika ya kiraia. Kwa mjibu wa ripoti ya shirika la habari la AFP iliyotolewa na msuluhishi wa Umoja wa Afrika Edem Kodjo inaelezwa kuwa makubaliano hayo yanatazamiwa kusainiwa leo Jumanne October 18, 2016 mjini Kinshasa na watu 300 walioshiriki katika mazungumzo.
Makubaliano hayo yaliyopitishwa katika kikao cha Jumatatu Oktoba 17, 2016 ni kuitaka Serikali kutekeleza masuala yafuatayo.
1. Tarehe ya uchaguzi
Hoja ya kwanza ya makubaliano yaliyofikiwa na vyama vinavyounga mkono serikali na upinzani ni kutotajwa tarehe ya uchaguzi wa urais, wabunge na wawakilishi wa majimbo. Tarehe pekee iliyotajwa ni tarehe ya kuwasilisha fomu za kugombea ambayo ni October 30, 2017.
Uchaguzi mkuu utafanyika ndani ya muda wa miezi sita ambayo ni wishoni mwa mwezi Aprili 2018, ndivyo wajumbe wa vyama vinavyunga mkono serikali na upinzani walivyoafikiana. Ingawa baadhi ya wajumbe wamekua wakijiuliza kama Tume ya Uchaguzi itaheshimu tarehe hiyo mpya.
2. Waziri mkuu kutoka chama cha upinzani
Hoja ya pili, Waziri Mkuu atateuliwa kutoka katika chama cha upinzani kilichoshiriki katika mazungumzo. Hakuna maelezo kuhusu kugawana nyadhifa katika serikali ya umoja wa kitaifa na Serikali itaundwa ndani ya siku 21 baada ya kusainiwa mkataba.
3. Kamati ya ufuatiliaji
Hoja ya tatu, kamati ya ufuatiliaji itakutana mwezi mmoja baada ya kusainiwa kwa mkataba: wajumbe saba kutoka vyama vinavyounga mkono serikali, wengine saba kutoka vyama wa upinzani na watatu kutoka vyama vya kiraia.
4. Ukomo wa utawala wa Rais Joseph Kabila
Hoja ya nne, Kuhusu hatma ya rais Joseph Kabila baada ya Desemba 19, imeelezwa kuwa Rais huyo ataendelea kubakia madarakani hadi atakapoapishwa Rais mwengine. Makubaliano hayo yanazungumzia juu ya kuzingatia Katiba.
Hata hivyo vyama vya upinzani ambavyo vinajumuika katika muungano wa “Rassemblement” pamoja na baadhi ya mashirika ya kiraia ambayo yalisusia mazungumzo hayo yametoa wito wa kumiminika mitaani Jumatano Oktoba 19.
Wakati hayo yakijiri, Tume ya Uchaguzi ya Congo (CENI) imeruhusiwa na Mahakama ya Katiba kuahirisha rasmi uchaguzi mkuu wakati ambao hali ya wasiwasi na hofu ya kutokea machafuko nchini DR Congo imeendelea kutanda.
ULIMISS TAARIFA YA MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU KUHUSU SERIKALI KUTENGA MABILIONI YA KUONDOA TATIZO LA UPUNGUFU WA MADAWA