Wiki moja baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwapa siku 7 Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Dar es Salaam Eng. Geofrey Mkinga na Mkurugenzi wa DAWASA, Lydia Ndibalema wawe wamekamilisha kipande cha barabara ya Mariki kinachoingia geti kuu la Muhimbili Hosp. kwa kiwango cha lami, tayari utekelezaji wa agizo hilo umekamilika tangu jana saa saba mchana na barabara hiyo imeanza kutumika.
Ripota wa @AyoTV_ , Bakari Chijumba amefika hadi eneo hilo na kuongea na Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilala, Eng. Sylvester Chinengo “Tulipokea maelekezo kutoka kwa Waziri Mkuu Jumatatu ya Wiki iliyopita kwamba tuharakishe kipande hiki cha barabara, tumepambana kuanzia Jumatatu usiku alipotoa agizo na kufikia jana Jumapili saa saba mchana tukawa tumekamilisha”
Barabara hiyo ambayo ilibomolewa kwa urefu wa mita 60 kupisha matengenezo ya bomba la maji machafu linalotoka katika Hospitali hiyo ilipaswa kuwa imekamilika mwishoni wa June mwaka huu ambapo Jumatatu July 24,2023 Majaliwa alishtukiza eneo hilo na kuwaagiza Watendaji hao kufanya kazi usiku na mchana ili kuepusha adha kwa Wagonjwa na Wanafamilia wanaoitumia barabara kuelekea Muhimbili Hosp.