Habari zilizosambaa tangu asubuhi kuwa Daraja la Dumila lililopo mkoani Morogoro ambalo ni barabara ya Dodoma – Morogoro limekatika na magari hayapiti baada ya mvua kubwa kunyesha usiku wa kuamkia leo.
Baadhi ya magari yatokayo upande wa Dodoma na Morogoro yameamua kugeuza na kurudi yalipotokea maana hakuna njia nyingine zaidi ya hiyo.
Kutokana na mvua hiyo madarasa katika Shule ya Msingi Magole, Dumila, Morogoro nayo yamefunikwa na maji na wanafunzi kuamua kujiokoa kwa kupita madirishani. Mpaka sasa hali bado si nzuri eneo hilo la Dumila wilayani Mvomero.
Taarifa iliyopo ni kwamba Serikali imeamua kuifunga hiyo barabara kwa muda.