Katibu Mkuu Wizara ya Maji Eng. Mwajuma Waziri amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda Sinohydro kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo na kuukamilisha kwa wakati ili kufikia malengo ya serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha inamaliza changamoto ya huduma ya maji katika mikoa yaMorogoro, Pwani na Dar es salaam.
Eng. Mwajuma ameyasema hayo katika ziara yake ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Bwawa hilo linalotarajia kuhifadhi maji kiasi cha mita za ujazo Milioni 190 pindi litakapo kamilika.
“Utekelezaji unaenda vizuri na juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinaonekana, fedha tayari zipo ni muda sasa wa mkandarasi kufanya kazi ili wananchi wanufaike na hili Bwawa la Kidunda” amesema
Katika ziara hiyo Eng. Mwajuma ameambatana na Kamishina wa Bajeti kutoka Wizara ya Fedha Bw. Meshack Anyingisye ambaye amekiri kufurahishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa Bwawa huku akiiomba Wizara ya Maji kuendelea kuweka uangalizi wa kutosha ili mradi huu uweze kukamilika kwa wakati.