Mkutano mkuu wa kwanza wa mwaka wa Mfuko wa Uwekezaji wa Faida (Faida Fund) utafanyika Agosti 10, 2024 mkoani Dar es Salaam.
Mkutano huo ni wa kwanza tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Faida unaolenga kutoa fursa kwa wawekezaji wote wa mfuko kupokea na kujadili taarifa ya fedha kwa kipindi cha mwaka unaoishia Juni 30, 2023.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investment (WHI) Dkt. Fred Msemwa amesema katika kipindi cha muda mfupi WHI kupitia Mfuko wa Faida imeweza kuweka msingi imara utakaowezesha kuziba ombwe la wawekezaji wadogo kushindwa kushiriki kwenye uwekezaji katika masoko ya fedha na kupata faida.
Amesema Mfuko wa Faida umeweza kufanya mambo makubwa ikiwemo kuwa mfuko wa kwanza Tanzania, kushusha kianzio cha kuwekeza kuwa angalau shilingi 10,000 na kuwawezesha wawekezaji wote hata wale wadogo kupata faida shindani na sawia katika soko.