Kwa mujibu wa gazeti la habari za michezo la Nchini Uturuki la Takvim limeripoti kuwa klabu ya Fenerbahce ya Uturuki inavutiwa na mshambuliaji mpya wa Aston Villa ya England, Mbwana Samatta.
Mshambuliaji huyo raia wa Tanzania alijiunga na Villa katika dirisha la usajili lililopita akiwa chaguo la kwanza ili kuziba pengo la Mbrazil, Wesley aliyekuwa akisumbuliwa na majeraha.
Samatta ameshindwa kuleta mafanikio ndani ya Aston Villa katika michezo yake ya Premier League baada ya kufunga goli moja 1 pekee katika michezo 12 aliyocheza.
Kwa mujibu wa Takvim, Fenerbahce inakaribia kumnasa Samatta kutokana na hali iliyopo kwa sasa ndani ya Aston Villa na itawakilisha ofa yake ya kumchukua kwa mkopo kutoka katika klabu hiyo ya Birmingham.
Inadaiwa yapo makubaliano ya maneno baina ya Samatta na Villa kuwa Aston Villa itatakiwa kumruhusu kujiunga na klabu nyingine endapo timu hiyo haitafanikiwa kuwepo Premier League katika msimu ujao.