Waziri wa Utamaduni wa Lebanon amesema filamu ya sinema ya “Barbie” inaeneza mawazo na fikra hatari na ni tishio kwa mfumo wa uumbaji.
Akizungumza katika mahojiano maalum na shirika la habari la Iranpress siku ya Jumapili, Mohammed Wissam Al-Mortadha ameeleza sababu ya kuzuia kuonyeshwa filamu ya “Barbie” nchini Lebanon kwa kubainisha kwamba filamu hiyo ni tishio kwa thamani na maadili ya Lebanon na ndiyo sababu ya kupigwa marufuku isionyeshwe nchini humo.
Waziri wa Utamaduni wa Lebanon ameongeza kuwa baada ya kuichunguza filamu ya “Barbie”, ilibainika kuwa kwa mtazamo wa kimaadili, maudhui ya filamu hiyo inahatrisha msingi wa familia na jamii ya Lebanon, na kwa sababu hiyo, ikatolewa amri ya kupiga marufuku kuonyeshwa filamu hiyo nchini humo.
Mohammed Wissam Al-Mortadha amebainisha kuwa filamu ya “Barbie” inaeneza fikra ya kuishi maisha ya ujane na ukapera na wakati huohuo inazungumzia ushoga na kwa sababu hiyo, inaharibu muundo wa familia unaojumuisha mwanamme na mwanamke.
Waziri wa Utamaduni wa Lebanon ameongeza kuwa,fikra zote hizo zinahatarisha uelewa wa vijana wa Lebanon, na katika hali kama hiyo, viongozi wote wa Lebanon walikuwa na wajibu wa kukabiliana na hatari ya filamu hiyo ya “Barbie”…/