Klabu ya soka ya Uturuki Galatasaray imemshutumu Jose Mourinho kwa kutoa “taarifa za kibaguzi”, ikisema kuwa itaanzisha kesi ya jinai dhidi ya meneja wa Fenerbahce kutokana na maoni yake kufuatia sare ya 0-0 ya timu hizo kwenye Super Lig.
Ingawa haijafahamika ni taarifa zipi ambazo Galatasaray alikuwa akirejelea, Mourinho alisema benchi la wenyeji lilikuwa “linaruka kama nyani” na kwamba mechi hiyo ingekuwa balaa ikiwa mwamuzi wa Uturuki angekuwa msimamizi.
Mchezo wa Jumatatu ulichezeshwa na mwamuzi wa Slovenia Slavko Vincic baada ya vilabu vyote viwili kuomba afisa wa kigeni kuchukua jukumu.
Galatasaray alisema kwenye X kwamba Mourinho “ameendelea kutoa kauli za dharau zilizoelekezwa kwa watu wa Uturuki” tangu aanze jukumu lake katika ligi.
“Leo, mazungumzo yake yameongezeka zaidi ya maoni machafu na kuwa maneno ya kinyama,” klabu hiyo ilisema.
“Tunatangaza rasmi nia yetu ya kuanzisha kesi ya jinai kuhusu kauli za ubaguzi wa rangi zilizotolewa na Jose Mourinho, na kwa hivyo tutawasilisha malalamiko rasmi kwa UEFA na FIFA.”