Uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) unathibitisha tukio la ajali lililotokea tarehe 19
Januari, 2022 maeneo ya Banana katika kivuko cha reli na barabara, ambapo gari la abiria aina ya ‘Coaster’ lenye namba za usajili T701 CKD linalofanya safari kati ya Tandika na Mbezi limegonga treni.
Ajali iliyotokea majira ya saa 11:10 jioni imehusisha Treni ya mjini inayotoa huduma ya usafiri wa abiria kati ya Kamata na Pugu jijini Dar es Salaam.
Katika ajali hii majeruhi ni abiria 6 waliokuwa wakisafiri na basi ambapo wanawake ni 3 na wanaume 3 na vifo vya wanawake 2, majeruhi wote wamepelekwa hospitali ya Amana kupatiwa matibabu.
Aidha, dereva wa basi alitahadharishwa kwa kupigiwa honi na dereva wa treni, hakuzingatia
na hata aliposimamishwa na mshika bendera dereva wa basi aliamua kukatiza reli na kupelekea ajali.
Uongozi wa Shirika la Reli Tanzania unaendelea kusisitiza Umma kuwa makini na kufuata
Sheria na taratibu zinazoonesha alama zilizopo katika vivuko vya reli na barabara na
kwamba dereva anapokaribia makutano anapaswa kupunguza mwendo na kusimama umbali wa mita 100 kuhakikisha endapo njia ni salama ili kuendelea na safari.
Shirika la reli Tanzania linatoa pole kwa abiria wote waliofikwa na ajali pamoja na kuwaombea majeruhi wapone mapema iliwa waweze kuendelea na shughuli za kujenga Taifa.