Serikali imelifunga na kulifutia leseni ya uchapishwaji na usambazaji wa gazeti la Tanzania Daima.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Patrick Kipangula ambaye amechapisha barua rasmi na kusema kuwa kuanzia Juni 24, 2020 gazeti hilo halitachapishwa wala kusambaza nakala zake hadi pale watakapojirekebisha na kuwa tayari kufuata taratibu, kanuni, sheria na maadili ya uandishi wa habari.
Hayo yamejiri ufuatia kukithiri na kujirudia kwa makosa yanayokiuka sheria za nchi na maadili ya uandishi wa habari.
Aidha, Serikali inaendelea kuvipongeza vyombo vingine vya habari kwa kutii sheria na kufuata misingi na taaluma ya uandishi wa habari kama sheria inavyoelekeza.