Siku chache baada ya mripuko wa volkano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kiwango cha gesi hatari kimeendelea kuongezeka katika baadhi ya maeneo ambako tope la moto la volkano hiyo bado linachemka.
Wakati huu ambapo shughuli zimeanza kurejea upya Mjini Goma kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la gesi inayotishia maisha ya wananchi ambao wamepakana na maeneo yaliyofunikwa na tope la volkano.
Siku ya Jumatatu (Mei 24), miili ya watu saba ilikutwa katika Kijiji cha Kibati mbali kidogo na Mji wa Goma, ambapo vyanzo vilieleza watu hao walikuwa wakijaribu kuvuka tope la moto kutoka kwenye volkano hiyo na kufariki kutokana na gesi.
Mkuu wa Taasisi ya Uchunguzi wa Milima ya Moto, Kasereka Mahinda, amethibitisha vifo hivyo akisema kuwa hali ilikuwa bado ni mbaya zaidi.
May 25,2021 wananchi walioathirika na mripuko huo wa volkano walikuwa bado hawajapatiwa msaada wowote, huku wengi wao wakiwa wamehifadhiwa na ndugu, jamaa na marafiki.