Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema hali ya maambukizi ya homa ya Mpox barani Afrika bado ni “ya wasiwasi mkubwa”, wakati idadi kubwa ya maambukizi inashuhudiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi na Uganda.
Kwa mujibu wa ripoti mpya ya WHO, hadi kufikia Desemba 15 Afrika ilikuwa imethibitisha maambukizi ya watu 13,769 katika nchi 20, na wagonjwa 60 kati yao wamefariki. DRC imeathiriwa zaidi ikiwa na watu 9,513 waliothibitishwa kuambukizwa.
Mlipuko mpya wa homa hiyo unatokana na kuibuka na kuenea kwa virusi vilivyobadilika aina ya clade 1b, ambavyo ni hatari zaidi na havijaeleweka vizuri, na viligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini DRC mwezi Septemba mwaka 2023.
Ingawa hali ya nchini DRC, ambayo ni kiini cha mlipuko huo, imetulia kwa kiasi katika wiki za karibuni, WHO imeonya kuwa mwelekeo wa sasa ya kupungua kwa maambukizi unatakiwa kutafsiriwa kwa umakini, kutokana na uwezekano wa kuchelewa kwa ripoti za maambukizi mapya.