Kundi la wanamgambo la Hamas Jumatano lilisema kwamba wapatanishi wake wamesisitiza utayari wake wa kutekeleza sitisho la vita la “mara moja” na Israel huko Gaza, kulingana na pendekezo la hapo awali la Marekani bila masharti ya kutoka upande wowote.
Kundi hilo lilisema katika taarifa kwamba timu ya wapatanishi wake, inayoongozwa na afisa mkuu Khalil al-Hayya, ilikutana na wasuluhishi Jumatano mjini Doha, wakiwemo waziri mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani na mkuu wa idara ya ujasusi ya Misri Abbas Kamel kujadili hali ya hivi karibuni huko Gaza.
Mazungumzo yalishindwa kufikia makubaliano ya kumaliza vita vya miezi 11. Suala la udhibiti wa njia ya Philadelphi, kwenye mpaka kati ya Gaza na Misri, ni kikwazo kinachozidi kujitokeza.
Mkuu wa idara ya ujasusi ya Marekani William Burns, ambaye pia ni mpatanishi wa Marekani kuhusu Gaza, Jumamosi alisema kwamba pendekezo jipya lenye maelezo ya kina kuhusu sitisho la mapigano litatolewa ndani ya siku kadhaa zijazo.