Hamas ilikabidhi miili ya mateka wanne kwa Chama cha Msalaba Mwekundu mapema Alhamisi ili kubadilishana na Israel kuwaachilia mamia ya wafungwa wa Kipalestina, siku chache kabla ya awamu ya kwanza ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza kumalizika.
Afisa wa usalama wa Israel alithibitisha kuwa Hamas ilikabidhi miili ya mateka hao kwa Shirika la Msalaba Mwekundu. Israel ilisema masanduku hayo yalitolewa kwa usaidizi wa wapatanishi wa Misri kupitia kivuko cha Israel na mchakato wa kuwatambua umeanza.
Wakati huohuo, msafara wa Msalaba Mwekundu ukiwa umebeba wafungwa kadhaa wa Kipalestina walioachiliwa huru waliondoka katika gereza la Ofer la Israel kuelekea mji wa Beitunia, Ukingo wa Magharibi, ambapo mamia ya watu waliokuwa wakimtakia heri walijibizana kulitazama basi hilo lilipowasili.
Marafiki na familia waliwasalimia wafungwa walioachiliwa, wakiwakumbatia na kupiga picha. Mwanamume mmoja aliyeachiliwa alitoa ishara ya ushindi akiwa amebebwa kwenye mabega ya wafuasi, huku umati ukiimba “Mungu ni Mkuu.” Wafungwa walioachiliwa walivalia fulana za Jeshi la Magereza la Israel ambazo baadhi yao walizivua na kuzichoma moto.
Saa chache baadaye, mabasi yaliyokuwa yamebeba mamia ya wafungwa wengine wa Kipalestina yaliwasili katika mji wa Gaza wa Khan Younis, huku baadhi ya wanaume wakibusu ardhini walipokuwa wakitoka kwenye mabasi hayo.
Israel ilikuwa imechelewesha kuachiliwa kwa zaidi ya wafungwa 600 wa Kipalestina tangu Jumamosi kupinga kile ilichokiita kutendewa kikatili kwa mateka wakati wa kukabidhiwa kwao na Hamas.