Harakati ya Mapambano ya Wapalestina, Hamas imekataa rasmi masharti mapya yaliyowekwa na Israel ya kuhitimisha usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.
Siku ya Jumapili, duru ya hivi punde ya mazungumzo yaliyofanyika katika mji mkuu wa Misri, Cairo ilikwama na wajumbe wa Israel na Hamas waliondoka bila kuafikiana.
Mambo muhimu ya kuzingatia katika mazungumzo yanayoendelea yaliyopatanishwa na Marekani, Misri na Qatar ni pamoja na uwepo wa Israel katika kile kinachoitwa Philadelphi Corridor, eneo nyembamba la urefu wa kilomita 14.5 kwenye mpaka wa kusini wa Gaza na Misri.
Ujumbe wa Israel umeripotiwa kupendekeza kupeleka tena vikosi vyake ndani ya Ukanda huo, huku wakidumisha uwepo wa kudumu katika vituo 12 vya kupelekwa, vingi vikiwa kaskazini mwa Ukanda huo, pamoja na mhimili wa Netzarim.
Hamas ilisema Israel imerudi nyuma kwenye ahadi ya Julai 2 ya kuondoa wanajeshi kwenye Ukanda huo na kuweka masharti mengine mapya, ikiwa ni pamoja na kuwachunguza Wapalestina waliofurushwa makwao wanaporejea kaskazini mwa eneo hilo lenye wakazi wengi zaidi wakati usitishaji vita utakapoanza.