Top Stories

Hatimaye Tito Magoti na wenzie wafikishwa Mahakamani

on

Afisa Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti (26) na mwenzake ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Tehama, Theodory Gyan (36), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matatu likiwamo la utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh. Milioni 10.

Magoti na mwenzake wamefikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega na Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, Faraja Nchimbi na Renatus Mkude.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Simon amedai kuwa washtakiwa hao wawili katika tarehe tofauti kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, 2019 ndani ya jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania kwa pamoja na watu ambao hawapo mahakamani kwa makusudi walishiriki makosa ya kiuhalifu ya kumiliki programu ya Kompyuta iliyotengenezwa mahususi kufanya kosa la jinai na kuwawezesha kujipatia kiasi cha Sh. Mil 17,354,535.

Katika shtaka la pili, Wakili Nchimbi amedai katika tarehe tofauti kati ya Februari mosi, 2019 na Desemba 17, 2019 ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam kwa pamoja washtakiwa hao na mengine ambao hawapo mahakamani walimiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kutenda makosa ya jinsi.

Naye Wakili Mkude amedai katika shtaka la tatu, Inadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, mwaka huu, ndani ya jiji la Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walijipatia jumla ya Sh. 17,353,535 wakati wakijua mapato hayo yametokana na madharia ya kosa la kushiriki genge la uhalifu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwakuwa Mahakama hiyo aina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi mpaka ipate kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mshataka nchini (DPP).

Upande mashtaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 7, 2020 itakapotajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili kutokuwa na dhamana.

UWEZO WA PEKEE MTOTO WA DARASA LA TATU ATUNGA KITABU KILICHOCHAPISHWA KWA MWANDIKO WAKE

Soma na hizi

Tupia Comments