Top Stories

Rais Samia aipongeza Mwanamke Initiative Foundation kwa juhudi za kumkomboa Mwanamke

on

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameipongeza taasisi ya Mwanamke Initiative kwa juhudi kubwa inazofanya katika kumkomboa Mwanamke wa kitanzania hususani katika upande wa elimu.
Pongezi hizo zimetolewa na Rais Samia katika uzinduzi wa taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) uliofanyika katika hoteli ya Golden Tulip Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Rais Samia amewapongeza sana MIF kwa kuweza kutazama changamoto ya ufaulu kwa watoto wa kike katika visiwa vya Zanzibar na kuja na suluhu ya kutaka kumaliza tatizo hilo ambapo takwimu zinaonyesha kumekua na ufaulu hafifu kwa watoto wa kike visiwani Zanzibar hali inayokwamisha maendeleo ya haraka kwa mtoto wa kike na jamii nzima kwa ujumla.
“Jambo linalofanya na wenzetu wa MIF ni jambo la kizalendo linalopaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali kwani sote tuna fahamu kuwa ukimwezesha Mwanamke umeiwezesha jamii nzima hivyo taasisi hii inakwenda kuikomboa jamii nzima kupitia juhudi ambazo inafanya kwa mtoto wa kike” alisema Rais Samia.
Rais Samia aliongeza kusema kuwa kuifungua MIF ni jambo moja laikini kutatua changamoto zilizopo ni jambo lingine, hivyo ameipongeza MIF kwa kuonesha nia ya dhati katika kutatua kama sio kumaliza changamoto zilizopo. Pia aliwashukuru Walimu wahitimu ambao bado hawajapata ajira kwa kujitoa na kuungana na MIF kujitolea kutoa mafunzo ya ziada kwenye kambi za wanafunzi wanao karibia kufanya mitihani yao, kwani hii imekuwa chachu ya kuongeza ufaulu visiwani Zanzibar.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu MIF, Fatma Mwassa alisema MIF kama taasisi, itajihusisha na ukombozi wa mwanamke kupitia uwezeshaji kielimu na afya na hata sekta ya kilimo. Aidha, MIF kupitia mpango mkakati wake wa miaka mitano inakusudia kuwa na kituo kitakachoshughulika na watu wenye changamoto za afya ya akili na ulemavu wa kiakili, eneo ambalo mara nyingi husahaulika na nguvu Nyingi kuwekezwa kwa watu wenye ulemavu wa viungo tu.
“Ni matamanio ya MIF kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi na kufanya kazi bega kwa bega  na wananchi wote ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na umaskini, ujinga na maradhi kupitia uwezeshaji wa wanawake” alisema Bi. Fatma ambae amekua Afisa Mtendaji Mkuu wa Kwanza wa Taasisi hiyo.
Pamoja na kuzinduliwa kwake, taasisi ya MIF tayari imefanikiwa kutekeleza miradi kadhaa ikiwemo kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi bora wawili wasichana ambao watasomeshwa mpaka pale watakapofika kikomo cha elimu yao. Sambamba na hilo MIF inatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 10 wanaoshika nafasi 10 za juu kupata masomo nje ya nchi (Scholarship) kwa wasichana. Mpaka sasa MIF imefanikiwa kuwapeleka wanafunzi zaidi ya 100 katika vyuo vya ufundi Tanzania Bara, lakini pia inakusudia kujenga vyoo 150 katika shule mbalimbali nchini ambavyo kati ya hivyo 75 vitajengwa Tanzania Bara.
Taasisi ya MIF inafanya kazi na wadau wengine mbalimbali ili kutimiza malengo yake na kupitia urabishi wake na mabenki  na taasisi nyingine binafsi, imeweza kukusanya kiasi cha shilling Bilioni 1.7 ambazo zitaelekezwa kwenye uendeshaji wa taasisi hii. Vilevile taasisi ya MIF imeingia mkataba na nchi ya falme za kiarabu (U.A.E) ambao hawa watatoa ufadhili wa takribani Bilioni 15 utakaokwenda kusaidia ujenzi wa kituo cha mafunzo cha Amali-VTC, kituo ambacho kitakwenda kutoa mafunzo ya amali kwa wahitimu 1,000 kila mwaka.
Naye Mwenyekiti na Mwanzilishi wa MIF, Mh. Wanu Hafidh Ameir ambae ni Mbunge wa Viti Maalum visiwani Zanzibar alisema tangu utotoni ilikua ni ndoto yake kuweza kutoa mchango kwa wenye uhitaji katika jamii na ndipo lilipoanzia wazo la kuanzisha taasisi ambayo itakwenda kutoa msaada kwa jamii bila kujali uwepo wake binafsi ambapo lengo la taasisi hiyo ni kuona watoto wengi wa kike wanamaliza shule, wanafaulu na kujiamini kuendeleza maisha yao.
“ Sisi kama MIF milango yetu ipo wazi kwa kila mtu ambae anataka kuwa sehemu ya harakati hizi za kumkomboa mtoto wa kike na watoto wote kwa ujumla na kuona kwamba hawaishii njiani katika ndoto zao za maisha bali wanakamilisha ndoto zao na kuwa na mchango kwa jamii zao na Taifa zima kwa ujumla,” aliongeza Wanu.
Sambamba na kuboresha elimu kwa wanafunzi, MIF inakusudia kuinua viwango vya ufundishaji kwa kuendesha mafunzo ya walimu walio kazini. Kupitia programu ya ‘MIF Fellows’, taasisi ya MIF inakusudia kuinua viwango vya ufaulu, hususan Zanzibar, kwa Elimu ya Sekondari kwa wanafunzi kupata usaidizi wa kuyapata maarifa kupitia walimu wasaidizi walio katika mpango wa ‘MIF Fellows’.
Aidha, Aidha, MIF inakusudia kuwasaidia wasichana waliokatiza masomo kutokana na sababu mbalimbali ili waweze kuendelea na masomo ya Ufundi na Sekondari kupitia Vyuo Vya Maendeleo ya wananchi (FDCs) na taasisi nyingine zenye kutoa mafunzo kama hayo, Bara na Visiwani

Soma na hizi

Tupia Comments