Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo amesema Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama imefanya operesheni katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro na Arusha na kufanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 200.5.
Akiongea leo Dar es salaam, Lyimo amesema “Tumekamata pia bangi kavu iliyokuwa tayari kusafirishwa gunia 978, bangi mbichi gunia 5,465, bangi iliyosindikwa (skanka) kilogramu 1.5, methamphetamine gramu 531.43, heroin kete 3,878, cocaine kete 138, mililita 3,840 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Pethidine pamoja na kuteketeza ekari 1,093 za mashamba ya bangi”
“Aidha, kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB) Mamlaka imezuia kuingia nchini jumla ya kilogramu 1,507.46 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya”
“Ukamataji huo uliofanyika kuanzia tarehe 25 Machi, 2023 hadi tarehe 19 Juni, 2023 unahusisha Watumiaji 109 wakiwemo Raia watatu wa kigeni, baadhi ya Watuhumiwa wamefikishwa Mahakamani na wengine wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani taratibu za kisheria zitakapokamilika”