Naibu kiongozi wa wapiganaji wa Hezbollah wanaooungwa mkono na Iran nchini Lebanon, Sheikh Naim Qassem amesema wapiganaji wake wako tayari kuwakabili wanajeshi wa Israeli iwapo wataanzisha mashambulio ya ardhini.
Katika hotuba yake ya kwanza tangu kuuawa kwa kiongozi wa kundi hilo Hassan Nasrallah katika shambulio la Israeli ameahidi kwamba wapiganaji wake wataendelea na malengo yao licha ya kutokuwepo kwa Nasrallah na makamanda wengine waliouawa.
Aidha amekana kwamba Israeli haijaharibu uwezo wake wa kijeshi kama na kwamba wataendelea na mapiganao.
Sheikh Naim vilevile ametangaza kwamba kundi hilo linaendelea na mchakato wa kumteua katibu mkuu wake mpya na kwamba watamtangaza katika siku zijazo.
Wapiganaji wa Hezbollah walianzisha mashambulio ya kuvuka mipaka dhidi ya Israeli siku moja kupita tangu wapiganaji wa Hamas watekeleze shambulio dhidi ya Israeli tarehe saba ya mwezi Oktoba, shambulio ambalo limechochea mapigano katika ukanda wa Gaza.