Mamlaka nchini Pakistan zimetangaza kufunga shule katika jiji kubwa la Karachi leo hii, kutokana na mvua kubwa na upepo mkali uliosababishwa na mgandamizo mkubwa wa hewa katika Bahari ya Kiarabu, ambao unaweza kugeuka kuwa kimbunga.
Sehemu za Karachi zimepokea mvua ya milimita 147 usiku mmoja, na Meya wa jiji hilo, Murtaza Wahab,kupitia Mtandao wa X aliwataka wakazi wa eneo hilo kuepuka harakati zisizo za lazima.
Mgandamizo huo mkubwa ulio karibu na Rann ya Kutch huko Gujarat, India, unatarajiwa kuwa kimbunga leo hii, na utaelekea kaskazini magharibi mwa Bahari ya Kiarabu katika siku mbili zijazo, kwa mujibu wa ofisi ya hali ya hewa ya India.
Mamlaka za Pakistan zimewaonya wavuvi na mabaharia kutokwenda baharini na kutoa tahadhari ya mafuriko mjini na mafuriko ya ghafla katika maeneo ya milimani katika siku zijazo.
Zaidi ya watu 28 wamefariki na takriban 18,000 wamehamishwa tangu Jumapili kutoka miji iliyo karibu na pwani ya Gujarat, kwa mujibu wa mamlaka za usimamizi wa majanga, huku mvua zaidi ikitarajiwa katika jimbo hilo kutokana na kimbunga kinachojengeka. Taarifa zinaeleza kuwa uundaji wa kimbunga katika Bahari ya Kiarabu ndani ya mwezi Agosti ni tukio adimu, na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1964.