Wenyeviti wa vyama vya Upinzani kutoka Chadema,Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha NCCR-Mageuzi, jana usiku March 21 mara baada ya hotuba ya Rais March walikutana ili kutoa kauli ya pamoja kutokana na hotuba ya ufunguzi wa Bunge kwa maelezo kuwa tayari Rais amevuruga mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.
Wakati viongozi hao wakikutana Mwenyekiti wa Chama cha DP Mchungaji,Christopher Mtikila alisema Rais ameingilia mchakato na kutoa maelezo jinsi ya kuandika Katiba.
Wakizungumza mara baada ya hotuba hiyo Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe,James Mbatia na Profesa Ibrahim Lipumba,walisema wameipokea kwa masikitiko makubwa hotuba hiyo.
“Tunakwenda kujadili hotuba ya Rais na tutatoa msimamo wetu,” alisema Mbowe.
Awali Katibu wa muda wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),Julius Mtatiro alisema Rais Jakaya Kikwete amevuruga mchakato wa Katiba, kwani walitarajia angetumia mamlaka yake kama Rais kuwaunganisha.
“Rais tulitarajia angeongea kama mkuu wa nchi, lakini amezungumza kama Mwenyekiti wa CCM na kutoa msimamo juu ya muundo wa Muungano jambo ambalo hatukulitegemea,” alisema Mtatiro.
Alisema kwa Rais kutoa msimamo ni sawa na mwongozo jambo ambalo limevuruga mchakato mzima.
Source:Mwananchi.