Mix

Huduma itakayomsaidia mkulima kujua mabadiliko ya hali hewa “itaongeza uzalishaji”

on

Kampuni inayongoza ulimwenguni kwa usambazaji wa mbolea na utengenezaji wa virutubisho vya mazao, YARA, leo imezindua programu ya kidijitali kwa ajili ya wakulima ijulikanayo kama Yara  FarmCare, ambayo inatoa taarifa sahihi za kilimo zinazostahili kutumiwa na mkulima, ikiwa na lengo la kuinua ufanisi katika kilimo, na kuchangia katika kujenga sekta ya kilimo inayojitegemea na wakati huohuo kuhakikisha kuwa wakulima wananufaika na uwekezaji wao.

Programu hii, ambayo inaweza kupakuliwa kwenye Google Playstore, imetengenezwa mahsusi kwa ajili ya kutatua changamoto zinazojitokeza kila mara katika shughuli za kilimo kama ufanisi, upatikanaji wa faida, mabadiliko ya hali ya hewa, ikizingatiwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, kikichangia asilimia 25 ya Pato la Taifa (GDP), kikiajiri zaidi ya asilimia 40 ya nguvukazi na asilimia 70 ya wakazi wa maeneo ya vijijini.

Akiongea katika hafla ya uzinduzi wa programu hiyo jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa YARA, Winstone Odhiambo, alisema kampuni ya Yara inatambua kuwa mabadiliko ya hali ya hewa ni changamoto inayowakabili wakulima misimu yote kwa sababu yana uwezo wa kupunguza kiwango cha uzalishaji wa mazao, na kama hiyo haitoshi, inaweza kusababisha ukame, vitu ambavyo vinapunguza pato halisi la  kaya mojamoja, kusababisha uhaba wa chakula na uwezo wa kifedha wa wakulima, ambao ni takriban asilimia 70 ya wakazi wa vijijini.  

Alisema kuwa FarmCare ni chaguo sahihi ambalo linampa mkulima fursa ya kunufaika na thamani halisi ya fedha yake kwenye kilimo, kwa kuwa program hii ina nyenzo nyingi za kutumia kama vile daktari wa mimea, taarifa za hali ya Hewa, kikokotoo cha mbolea, maelekezo sahihi sawa na ambayo angetoa bwana shamba kwa kila hatua, na hivyo kuwasaidia wakulima  kuzalisha mazao bora zaidi ambayo nayo yanaongeza kiwango cha uzalishaji kwa eneo lilelile.

“ Wakulima wanahitaji kuwa na msimamizi wa karibu kila siku, mshauri, na mshirika ambaye anawahakikisha kuwa wanazalisha kitaalamu zaidi,wanatumia njia sahihi za kilimo, ili kuondoa dukuduku lao. Wanahitaji mbia awe nao muda wote, mtu ambaye wanaweza kumtegemea kuwapatia suluhisho la matatizo na changamoto zao ili wajipatie fedha zaidi, wapunguze matumizi wakati wa uzalishaji, yaani kwa lugha nyingine wavune mazao mengi kwa kuwekeza kidogo zaidi,”alisema Mkurugenzi Mtendaji Winstone Odhiambo.

FarmCare ni programu ya kidijitali ambayo inagusa maswala mtambuka ya kilimo, iliyosanifiwa maalum kuhakikisha kuwa mkulima wa Tanzania anakuwa si bora mkulima bali mkulima bora haswa. Kwa kubonyeza tu vitufe vya simu janja, wakulima wanajipatia ushauri bora kabisa wa wakati wa kupanda, ikiwa imesheheni elimu ya uhakika ya kilimo na mbinu nyingi za kuinua ufanisi wa kilimo kama shughuli. FarmCare ni nyenzo sahihi ya kilimo ambayo ina uwezo wa kufanya mabadiliko kwenye sekta ya kilimo Tanzania na kukifanya kilimo kuchukua nafasi na hadhi yake stahili kama msingi madhubuti wa uchumi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Huduma za Kidijitali kwa Wateja, Deodath Mtei, alisema “ Yara imeitikia kilio cha wakulima kwa wakati muafaka kwa kuzindua FarmCare, ambayo ina manufaa lukuki  ikiwemo elimu elekezi ya kilimo kupitia video, orodha ya namna ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya kilimo na utabiri wa hali ya hewa. Ina nyezo mbalimbali zenye lengo la kusaidia uzalishaji kama daktari wa mimea, , kipimo cha mbolea, ramani ya shamba, na kitufe cha kutambua maduka ya pembejeo za Yara yalipo. FarmCare ni program ambayo siyo tu inamsaidia mkulima, bali inatoa zawadi na kuponi kwa njia ya mashindano.”

Program ya FarmCare imezinduliwa ikilenga kuwa mwenza wa mkulima na nyenzo ya uhakika ya kidijitali ya kutoa suluhisho mbalimbali za kilimo, iliyosheheni taarifa na utalaamu wa hali ya juu ambayo mkulima anaweza kuirejea wakati wowote anapohitaji kutatua changamoto za kila siku za shughuli za kilimo msimu mzima.

Soma na hizi

Tupia Comments