Wajumbe wa bodi ya klabu ya Al Ahly wamependekeza kwa Rais wa klabu hiyo Mahmoud El Khatib kujaribu kumsajili mchezaji wa Al Nassr na Timu ya Taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo kwa mkataba wa mkopo wa miezi sita kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia la Klabu yatakayofanyika nchini Marekani.
Nahodha huyo wa Ureno atamaliza mkataba wake na klabu yake ya sasa ya Al Nassr ya Saudia Arabia tarehe 30 june 2025 ambayo haishiriki michuano hiyo ya Kombe la Dunia la klabu itakayoanza kutimua vumbi june mwaka 2025.
Mwekahazina wa klabu ya Al Ahly Khaled Mortagy akizungumza usiku wa jana kwenye TV ya klabu hiyo amesema hakuna kikomo cha fedha kwa usajili wowote ndani ya klabu hiyo na mchezaji yeyote atakayehitajika na kocha wao Marcel Koller watampata.
“Hakuna kikomo cha fedha kwa usajili wowote ndani ya Al Ahly mchezaji yeyote atakayehitajika na kocha tutampata,tunaujasiri kuelekea Kombe la Dunia la klabu”.
Akizungumzia tetesi juu ya usajili wa nyota huyo wa zamani wa Real Madrid kiongozi huyo wa Al Ahly amesema inaweza kuwa ngumu lakini maamuzi yanabaki mikononi mwa Rais wa klabu hiyo.