Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipoteza fursa ya kufikia makubaliano ya kubadilishana mateka na Hamas mwezi Julai ili kuwaridhisha washirika wake wa muungano wa siasa kali za mrengo wa kulia Waziri wa Usalama wa Taifa Itamar Ben-Gvir na Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich, Shirika la Utangazaji la Umma la Israel KAN liliripoti.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Hamas ilikuwa tayari kuwaachilia mateka kadhaa wa Israel bila kutaka kusitishwa kikamilifu kwa mapigano hayo. Ripoti hiyo ilipendekeza kuwa nia ya Hamas wakati huo ilikuwa ni jaribio la kuunganisha awamu ya kwanza na ya pili ya pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano ambalo lilijumuisha misaada ya kibinadamu.
Ripoti hiyo haikutoa maelezo zaidi, hata hivyo, ingawa Hamas imesema mara kwa mara kwamba itawaachilia tu mateka wa Israel ikiwa makubaliano hayo yatasababisha kusitishwa kabisa kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza.
Wakati huo, pendekezo la Marekani lilijumuisha awamu tatu: ya kwanza ilihusisha usitishaji mapigano mara moja; kuachiliwa kwa wanawake, wazee na mateka wa Israeli waliojeruhiwa; na kubadilishana wafungwa pamoja na kuondolewa kwa majeshi ya Israel kutoka maeneo yenye watu wengi ya Gaza.
Ilijumuisha pia kuongeza misaada ya kibinadamu, kujenga upya huduma za kimsingi na kuwezesha kurejea kwa raia kwenye makazi yao kote Gaza.
Awamu ya pili ilihitaji kuachiliwa kwa mateka wote waliosalia na kuondolewa kabisa kwa vikosi vya Israel kutoka Gaza, kwa lengo la kumaliza mgogoro huo kwa uhakika
Awamu ya tatu ilihusisha ujenzi wa Gaza kwa miaka kadhaa na kurejesha mabaki ya wanajeshi wa Israel.