Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Kuu ya Dar es Salaam leo imeshindwa kutoa hukumu ya kesi ya kikatiba dhidi ya Kamishna wa Magereza Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) wote kutoka Chadema kutokana na Majaji kuwa katika vipindi vingine vya Kimahakama.
Kesi hiyo namba 13 ya mwaka 2021 ilifunguliwa katika Mahakama hiyo ambapo wawili hao wanapinga ukiukaji wa haki zao za msingi na kikatiba wakati wanatumikia adhabu walizopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya.
Nje ya mahakama, Ayo Tv na Millardayo.com imezungumza na Wakili wa walalamikaji hao, Charles Tumaini ambaye amesema kesi imeahirishwa hadi Disemba 19, 2022.
“Leo tumeambiwa Majaji wanavipindi vingine lakini kesi imeahirishwa hadi Disemba 19, ambapo tunatarajia hukumu hiyo itasomwa na Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Luvanda,”.
Miongoni mwa hoja nyingine wanazolalamikia ni utaratibu wa viboko kwa wafungwa wanaokutwa na hatia pamoja na wakulazimishwa kutotumia sehemu za haja kubwa mpaka pale watakapopata ruhusa kutoka kwa askari wa gereza jambo ambalo alisisitiza kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu.