Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas ilisema Alhamisi zaidi ya Wapalestina 30,000 wameuawa huko Gaza tangu vita kati ya kundi la wanamgambo na Israel kuanza karibu miezi mitano iliyopita.
Wakati wapatanishi wakisema makubaliano ya mapatano kati ya Israel na Hamas yanaweza kuwa yamesalia siku chache tu, mashirika ya misaada yametoa tahadhari ya njaa inayokuja kaskazini mwa Gaza.
Watoto wamekufa “kutokana na utapiamlo, upungufu wa maji mwilini na njaa iliyoenea” katika hospitali ya Al-Shifa ya Gaza City, ilisema wizara ya afya, ambayo msemaji wake Ashraf al-Qudra ametoa wito wa “hatua za haraka” kutoka kwa mashirika ya kimataifa ili kuzuia zaidi ya vifo hivi.
Akitoa mfano wa hali mbaya ya Gaza, mkuu wa USAID Samantha Power alisema Israel inahitaji kufungua vivuko zaidi ili “msaada wa kibinadamu unaohitajika sana uweze kuongezeka kwa kasi.”
“Hili ni suala la maisha na kifo,” Power alisema kwenye video iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii wa X.