Idadi ya watu waliofariki kutokana na maporomoko katika eneo la kutupata taka jijini Kampala imefikia watu 25, hatua inayokuja wakati huu matumaini ya kuwapata manusura zaidi yakiendelea kufifia kwa mujibu wa mamlaka nchini Uganda.
Mkasa huyo ulitokea Jumamosi ya wiki iliopita katika wilaya ya Kiteezi Kaskazini mwa jiji kuu la Kampala nchini Uganda, baada ya kutokea kwa maporomoko ya ardhi katika eneo la kutupia takataka kwa sababu ya mvua kubwa.
Watu na mifugo waliripotiwa kufunikwa kwenye takataka wakati wa tukio hilo ambapo kwa mujibu wa Waziri wa majanga nchini Uganda, Lillian Aber kufukia Jumatatu jioni, miili 25 ilikuwa imepatikana bila ya kuwepo kwa manusra.
Mvua kubwa imeripotiwa kuathiri shughuli za kupata miili zaidi kwenye eneo hilo, Rais Yoweri Museveni akiwa ametoa agizo kwa jeshi kusaidia katika zoezi la utafutaji wa watu walionaswa kwenye takataka.
Uganda na maeneo mengine ya Afrika Mashariki yamekumbwa na mvua kubwa hivi majuzi. Maporomoko ya udongo kusini mwa Ethiopia mwezi uliopita yakisababisha vifo vya takriban watu 250.