Watumishi wa Afya Halmashauri ya Mji wa Njombe wametakiwa kutowatoza fedha wagonjwa kwa ajili ya kulipia gari la kubebea wagonjwa kwani tayari Serikali imeshagharamia hivyo wagonjwa wanatakiwa kubebwa bure.
Kauli hiyo imetolewa Disemba 8,2024 na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Jabir Juma wakati wa hafla ya kukabidhi gari la kubeba wagonjwa katika kituo cha afya cha Ihalula kilichopo kata ya Utalingolo Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Amesema isijekutokea wananchi wakalalamika kuhusu kutozwa fedha kwa ajili ya gharama za kusafirisha wagonjwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kupata matibabu wakati serikali imetoa gari hilo bure ili kuboresha huduma kwa wananchi.
“Tusije tukaanza kulalamika watumishi hatufanani inawezekana siku moja akaingia tamaa au kushawishika na kuomba hela ya mafuta atakuwa ameteleza lakini mwananchi jua usafiri ni bure” amesema Juma.
Amesema Halmashauri hiyo italitunza gari hilo na kulifanyia matengenezo pale inapotakiwa kufanya hivyo na kuahidi kulipangia bajeti ya mafuta na vitu vingine vinavyohusu gari hilo la kubeba wagonjwa.
Amewaasa wananchi kutumia usafiri huo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwa gari hilo litabeba wagonjwa ambao wapo katika hali mbaya na wanatakiwa kupelekwa rufaa kwa matibabu zaidi.
Mganga mfawidhi wa kituo Cha Afya Ihalula Dk. Happiness Kwilasa amesema ujio wa gari hilo utasaidia kupunguza adha kwa wananchi ambao Wamekuwa wakitumia gharama kubwa kusafirisha wagonjwa pindi wanapopewa rufaa.
Amesema pamoja na ujio wa gari hilo la wagonjwa katika kituo hicho cha afya lakini Bado kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa wataalamu na miundombinu hasa nyumba za kuishi.
“Tuna uhaba wa watumishi katika kituo chetu hii hupelekea kukosekana kwa huduma kwa muda muafaka na haraka” amesema Kwilasa.
Mbunge wa Njombe Mjini Deo Mwanyika amesema zaidi ya Sh. 2 bilioni zimetengwa ili kujenga vituo vya Afya katika Halmashauri ya mji wa Njombe na lengo ni kupunguza changamoto za kukosekana kwa huduma za Afya kwa wananchi.
“Tumejenga vituo vitano vya afya katika vituo hivyo vinne vimejengwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya mji wa Njombe na kituo kimoja cha Luponde kinajengwa kwa fedha za serikali za tozo” amesema Mwanyika.
Diwani wa kata ya Utalingolo Erasto Mpete ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Erasto Mpete amewataka wananchi kulitunza gari hilo ili liwasaidie pamoja na vizazi vijavyo.
“Magari haya sehemu nyingine yamekuwa yakitumika sivyo hivyo wananchi mtoe taarifa mnapoona matumizi tofauti” amesema Mptete.
Mkazi wa kijiji cha Ihalula Agnes Mbilinyi amesema wamekuwa wakihangaika pindi wanapokuwa na mgonjwa hasa nyakati za usiku lakini ujio wa gari hilo utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo.
“Hatuna la kusema tunamshukuru mbunge wetu kwani ujio wa gar hili tutaokoa wagonjwa wetu wengi” amesema Mbilinyi.