Mwaka wa 8 wa vita dhidi ya Yemen umemalizika huku takwimu zikionyesha kuwa, kwa wastani, mtoto mmoja wa Yemen anafariki dunia kila baada ya dakika 10 katika vita hivyo.
Vita dhidi ya watu wa Yemen vilianza Machi 26, 2015, na sasa vimekamilisha mwaka wa nane huku vita hivyo vikitajwa na Umoja wa Mataifa kuwa maafa makubwa zaidi ya binadamu katika karne ya 21 na watoto ni miongoni mwa wahanga wakuu wa vita vya Yemen.
Shirika la haki za binadamu la “Intisaf” linalofanya kazi katika uwanja wa haki za wanawake na watoto, lilitangaza katika ripoti mwishoni mwa Februari 2023 kwamba katika siku 2900 za vita huko Yemen, wanawake na watoto elfu 13, 482 wameuawa au kujeruhiwa kama matokeo ya uvamizi wa Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya nchi hiyo.
Ripoti hiyo ilisema, zaidi ya wanawake milioni nane wanahitaji huduma za kuokoa maisha yao, na watoto milioni 12.6 wanahitaji aina fulani ya misaada ya kibinadamu.
Mwishoni mwa mwaka wa nane wa vita vya Saudia na washirika wake nchini Yemen, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeeleza wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya watoto milioni 11 nchini humo na kuonya kuwa, kwa wastani, mtoto mmoja wa Yemen hufariki dunia kila baada ya dakika 10 kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika.
UNICEF ilitangaza katika taarifa yake kwamba hivi sasa zaidi ya watoto 540,000 walio chini ya umri wa miaka mitano nchini Yemen wanasumbuliwa na “utapiamlo mkali na wa kutisha”.
Baadhi yao wamepata ulemavu wa viungo kutokana na kushambuliwa moja kwa moja, huku wengine wakiacha masomo na kwenda kufanya kazi ili kujikimu kimaisha baada ya wazazi wao kukatiwa mishahara.
Watoto wengine wa Yemen wamepatwa na maradhi ya aina mbalimbali kutokana na ukosefu wa chakula na dawa kunakosababishwa na mzingiro wa Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya nchi hiyo.