Bodi ya Filamu Tanzania imeridhishwa na ubora wa kazi za wasanii mikoani huku ikifurahishwa na mwamko wa wasanii kukabidhi kazi zao kwa bodi kwa ajili ya kuwania tuzo za filamu.
Akifafanua namna wasanii wanavyojitokeza na kuwasilisha kazi zao katika kampeni ya mtaa kwa mtaa zitakazokwenda kuwania tuzo katika tamasha la tuzo za filamu mwaka wa 2022,Benson Mkenda kaimu meneja wa kitengo cha utayarishaji kutoka bodi ya filamu amesema wamebaini uwepo wa kazi nzuri za wasanii katika maeneo ya mikoani zitakazoendelea kuleta ushindani mkubwa kwenye tuzo.
Aidha Bodi imetoa rai kwa watayarishaji wa filamu mkoani Njombe kutumia fursa ya kipekee ya utajiri wa vivutio kutengeneza filamu zenye maudhui za utalii ili kutengeneza fedha nyingi kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkenda ametoa rai hiyo mkoani Njombe wakati wa zoezi la kukusanya Filamu mtaa kwa mtaa kwa watayarishaji wadogo na wakubwa huku lengo likiwa ni kuziingiza kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo za filamu zinazotarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwaka huu.
Mkenda amesema wakati umefika kwa watayarishaji wa filamu nchini kuchangamkia fursa ya uwepo wa vivutio vingi vya utalii ikiwemo Milima,Bahari,Mapango ya kihistoria na vinginr vingi kuandaa filamu za tofauti ambazo zitavutia wageni kuja nchini kutembea.
Kwa mujibu bodi ya filamu inaelezwa takribani vibali 160 hutolewa kila mwaka kwa watayarishaji wa kigeni kuja nchini kutayarisha filamu katika maeneo tofauti ya vivutio na kwamba kitendo cha kupata filamu 10 katika mkoa wa Lindi,Mtwara 21 na Ruvuma 25 kimeonyesha mwamko umeanza kukua katika tasnia hiyo.
“Tunapita mtaa kwa mtaa kukusanya filamu kutoka kwa watayarishaji na kisha kuziingiza kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ,hatua ambayo itasaidia kuongeza hamasa kwa wazalishaji kuongeza bidii na ubunifu,Alisema Benson Mkenda kaimu meneja wa kitengo cha utayarishaji bodi ya filamu Tanzania”
Baadhi ya wasanii waliyojitokeza katika mkoa wa Njombe kuwasirisha filamu zao katika bodi ya filamu ili ziingie kwenye mchujo akiwemo Happy Mwesi alimaarufu Angel Kidoti wanasema kitendo kilichofanywa na wizara kupitia bodi ya filamu kwasasa kimewapa ari ya kuongeza ubunifu ili kuzalisha maudhui bora na yatakayokidhi mahitaji ya dunia.
Wameongeza kuwa mwanzo walikuwa wanapata shida kuzifikia mamlaka kwa kulazimika kupanda gari hadi Dar es salaam lakini kitendo cha kufuatwa mitaani kinawapa nguvu.