Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisema jana kwamba Tehran huenda ikaelekea kwenye umiliki wa silaha zake za nyuklia ikiwa nchi za Magharibi zitaendelea na tishio la kurejesha vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa.
Araghchi aliwaambia waandishi wa habari kwamba Iran hapo awali ilikuwa na uwezo na ujuzi wa kutengeneza silaha za nyuklia, lakini hii haikuwa sehemu ya mkakati wa usalama wa nchi.
“Ikiwa nchi za Ulaya zitaiwekea tena vikwazo Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kila mtu nchini Iran atashawishika kuwa kanuni ya kutomiliki silaha za nyuklia ni mbaya,” aliongeza.
Maafisa wa Iran wanatarajiwa kukutana na manaibu mawaziri wa mambo ya nje kutoka Uingereza, Ujerumani na Ufaransa mjini Geneva leo kujadili mpango wa nyuklia wa Tehran na maendeleo ya kikanda.
Araghchi alisema kikao cha kujadiliana kinalenga kuona kama kuna njia ya kutoka katika hali ya sasa.