Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Iringa, ulio katika Kata ya Nduli, Mkoani Iringa, umefikia asilimia 93 ya ukamilifu na umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 68.
Kwa sasa, uwanja huo uko tayari kwa matumizi, huku safari za ndege kubwa zikitarajiwa kuanza rasmi tarehe 22 Februari 2025.
Hayo yamebainishwa leo, Februari 7, 2025, wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo ,Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, amesema kuwa uwanja huo utaanza kupokea ndege kubwa, ikiwa ni pamoja na ndege ya aina ya Bombardier.
“Ujenzi huu wa kisasa utafungua milango ya maendeleo kwa uchumi wa lringa pamoja na uchumi wa nchi yetu, kwani utaongeza idadi ya watalii na shughuli nyingine za kiuchumi,” alisema Mbarawa.
Waziri Mbarawa ameeleza kuwa zamani wageni walikuwa wakitoka Zanzibar na kwenda moja kwa moja kwenye mbuga za wanyama, lakini sasa wataweza kutumia uwanja huu kuja Iringa na kuendelea na shughuli zao za utalii.
“Zamani, usafiri wa ndege kutoka Dar es Salaam hadi Iringa ulikuwa unafanyika kwa ndege ndogo, na gharama yake ilikuwa shilingi laki 700,000.
Hata hivyo, kutokana na ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya uwanja huu, sasa abiria wataweza kusafiri kwa gharama ya shilingi laki 250,000 hadi laki 300,000.”Alisema Waziri
Hata hivyo kukamilika kwa uwanja huu, Iringa Kwa sasa itakuwa na fursa ya kuongeza usafiri wa ndege na kuhamasisha ukuaji wa sekta mbalimbali za kiuchumi katika mkoa hapa.