Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema, Israel tayari imempiku kiongozi wa Wanazi Adolf Hitler kwa kuua zaidi ya watoto 14,000 wasio na hatia katika Ukanda wa Ghaza.
Erdogan ameyasema hayo alipohutubia mkutano wa wabunge wa chama chake cha Uadilifu na Maendeleo (AK) na kubainisha kuwa, kwa uungwaji mkono usio na masharti kutoka Magharibi, Israel inafanya mauaji ya halaiki huko Ghaza na Ukingo wa Magharibi yanayoacha alama za kutia aibu katika historia ya wanadamu.
Rais wa Uturuki ameendelea kueleza kwamba, hakuna anayeweza kuhoji jinsi Uturuki inavyoguswa na suala la Palestina, na akaongezea kwa kudai kuwa kadhia ya Palestina imeyapa maisha yake yeye maana mpya.
“Mungu akinijalia uhai, nitaendelea kutetea mapambano ya Palestina, na nitakuwa sauti ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina,” amesema Erdogan.
Akilinganisha mapambano ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestia HAMAS dhidi ya Israel na Vita vya Kupigania Uhuru vya Uturuki vya zaidi ya miaka 100 iliyopita, Erdogan ameongezea kwa kusema: “Tunafahamu vyema kwamba kuna gharama ya kulipa kwa kutamka haya”.